Waziri Mkuu wa China atoa wito kwa juhudi za kutatua matatizo yanayozikabili nchi zinazoendelea
2023-06-24 11:10:26| cri

Katika kukabiliana na pengo la ufadhili wa maendeleo duniani, China imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana kwa dhati na kufanya kazi pamoja kutatua matatizo yanayoozikabili nchi zinazoendelea, hasa nchi dhaifu.

Hayo yamesemwa na waziri mkuu wa China Li Qiang katika hotuba yake aliyoitoa siku ya Ijumaa kwenye hafla ya kufungwa kwa Mkutano wa Mkataba Mpya wa Ufadhili Duniani, ambao uliongozwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na kuhudhuriwa na zaidi ya wakuu 60 wa nchi, serikali, na mashirika makubwa ya kimataifa.

Bw. Li ametoa pendekezo la mambo matatu katika suala hili. Kwanza, kuendeleza kwa uthabiti mageuzi ya usimamizi wa mambo ya fedha duniani na kujenga mazingira bora ya ufadhili kwa nchi zinazoendelea. Pili, kujenga uhusiano wa wenzi wa maendeleo wa kimataifa na kutoa rasilimali zaidi za maendeleo kwa nchi zinazoendelea. Tatu, kuendeleza kwa uthabiti mwingiliano wa kiuchumi na biashara huria ili kuingiza msukumo mpya wa ukuaji katika nchi zinazoendelea.

Li amesisitiza kuwa katika dunia hii inayojaa mizozo na sintofahamu, China na Ulaya zinapaswa kutafuta muafaka huku zikiweka kando maoni tofauti, kupanua maelewano huku zikipunguza mifarakano, kuendeleza ushirikiano  katika uvumbuzi, kukabiliana na hali ya kimataifa yenye sintofahamu kwa utulivu wa uhusiano kati ya China na Ulaya, na kukuza kwa pamoja maendeleo endelevu ya binadamu.