Bwana Yevgeny Prigozhin akomesha uasi nchini Russia
2023-06-25 12:43:52| CRI

Tajiri wa Russia Yevgeny Prigozhin amekomesha uasi wa kundi lake la mamluki la Wagner dhidi ya Russia, kwenye makubaliano yaliyosimamiwa na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus.

Msemaji wa Ikulu ya Russia Bw. Dmitry Peskov amesema, serikali ya Russia itaondoa mashtaka ya uhalifu dhidi ya Prigozhin na "atakwenda Belarus", na kuwa wanajeshi wa Wagner hawatakabiliwa na mashtaka. Rais Vladimir Putin wa Russia amemshukuru Bw. Lukashenko kwa kufanikisha makubaliano hayo.

Vikosi vya Wagner vilikuwa vimefika katika jiji la Lipetsk, takriban kilomita 450 kusini mwa Moscow, kabla ya Prigozhin kuamuru kila askari kurudi kambini. Bw. Prigozhin na wanajeshi wengine wa Wagner walionekana wakiondoka katika makao makuu ya jeshi katika wilaya ya Rostov-on-Don, ambayo walikuwa wameyateka.

Prigozhin alianza uasi Ijumaa baada ya kulishutumu jeshi la Russia kufanya shambulizi la kombora dhidi ya wanajeshi wake nchini Ukraine, lakini Russia ilikanusha shutuma hiyo. Wakati hali ya wasiwasi ikipungua nchini Russia, Kremlin imetangaza kuwa itamaliza operesheni ya kukabiliana na ugaidi ambayo iliweka askari na magari ya kijeshi katika mitaa ya mji wa Moscow.