Wanawake Tanzania watakiwa kuchangamkia fursa kwenye ubaharia
2023-06-26 19:35:54| cri

Takwimu zilizopatikana hivi karibuni nchini Tanzania zinaonesha kuwa idadi ya mabaharia waliopo Tanzania kwa sasa ni takribani 9,000, huku wanawake wakiwa ni chini ya asilimia moja ya idadi hiyo.

Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya Ilemela (DC), Bw. Hassan Masala, wakati akifunga maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, yaliyoratibiwa na Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC). Bwana Masala amewashauri wasichana kujikita katika masomo ya ubaharia, sio tu kuziba pengo la ubaharia kijinsia, bali kuchangamkia fursa zilizomo katika sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji.

Amesistiza kwamba sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji ina fursa nyingi kiuchumi, kwani asilimia 90 ya biashara zote za kimataifa duniani husafirishwa kwa njia ya meli.