Bunge la Afrika Mashariki lazuia matumizi ya Kiswahili katika vikao vyake
2023-06-26 21:35:03| cri

Lugha ya Kiswahili ambayo hivi karibuni ilifanywa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wiki iliyopita ilizuiwa kutumika kwenye mkutano wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutokana na wabunge kutoka baadhi ya nchi wanachama kutoruhusu matumizi yake, wakisisitiza kuwa Kiingereza kiendelee kuwa lugha ya kazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Sakata hilo lilikaribia kuwagawa wabunge hao, na lilianza wakati mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka DRC alipokuwa akijadili hoja kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi nchini Uganda.

Akitoa mchango wake kuhusu mauaji ya kikatili magharibi mwa Uganda Bibi Dorothe Masirika Ngana, aliomba kubadilisha lugha ya kikazi kutoka kiingereza na kutumia Kiswahili, ombi lake lilipingwa vikali na wabunge wenzake.

Hoja ya mbunge kutoka Sudan Kusini Bw. Gabriel Alaak Garang alipata ushindi baada ya kusema kuwa kiingereza ndiyo lugha ya kikazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, alionya kuwa kuruhusu Kiswahili kutumika katika bunge la Afrika Mashariki kunaweza kukaribisha changamoto mpya, kama vile Sudan Kusini inaweza kupendekeza kutumika kwa lugha ya kiarabu.