Waziri mkuu wa China akutana na wakuu wa WTO na WEF
2023-06-27 08:40:05| CRI

Waziri Mkuu wa China Li Qiang jumatatu kwa nyakati tofauti amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ngozi Okonjo-Iweala  na mwenyekiti wa Baraza la Uchumi Duniani (WEF) Klaus Schwab.

Katika mazungumzo na Bi. Okonjo-Iweala, Li Qiang amesema China inapenda kushirikiana na pande zote, kuunga mkono utaratibu wa pande nyingi na biashara huria, huku ikipinga utaratibu wa upande mmoja na kujilinda kibashara, pia kuhimiza mageuzi ya WTO kupata maendeleo mapya, na kulinda hadhi ya njia kuu iliyowekwa chini ya mfumo wa biashara ya pande nyingi.

Kwa upande wake, Bi. Okonjo-Iweala amesema WTO inatarajia kujenga uhusiano wa kiwenzi wenye nguvu na China, ili kuchangia katika kuhimiza mageuzi ya shirika hilo na kulinda mfumo wa biashara ya pande nyingi.

Alipokutana na Schwab, Li Qiang amesisitiza kuwa China itashikilia kithabiti njia ya kujiendeleza kwa amani, kufungua mlango zaidi, kushirikiana na pande mbalimbali kujenga uchumi wa dunia ulio wazi, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Naye Schwab amesema, WEF inapenda kuimarisha uhusiano wa kiwenzi na China, kuhimiza pande mbalimbali kukabiliana kwa pamoja changamoto mbalimbali duniani ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ili kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.