Ethiopia na China zimezindua Kituo cha Pamoja cha Utafiti na Upanuzi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ili kuongeza kasi ya maendeleo ya nishati safi nchini Ethiopia.
Kituo hicho kinatarajiwa kutumika kama jukwaa la utafiti, mafunzo na majaribio ili kuboresha uwezo wa kupata teknolojia za nishati safi na kuwezesha kutimiza Ajenda ya Mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Maji na Nishati wa Ethiopia Sultan Wali, amesisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Nchi hiyo, China na UNDP katika utafiti wa rasilimali za nishati safi.
Naibu mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Usimamizi wa Ajenda 21 cha China, Chen Qizhen amesema, licha ya changamoto na sintofahamu inayoikumba dunia kwa sasa, mfumo wa ushirikiano wa Kusini – Kusini unaendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi.
Naye naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Ethiopia, Cleophas Torori amesema, kama sehemu ya juhudi za kuondoa pengo la upatikanaji wa nishati na kutimiza malengo ya nishati na mabadiliko ya tabianchi nchini Ethiopia, UNDP, kwa kushirikiana na China, inaunga mkono serikali ya Ethiopia katika kutekeleza ushirikiano wa Kusini – Kusini, huku ikilenga katika mradi wa pande tatu wa ushirikiano wa nishati safi.