Rais Mwinyi ainadi Zanzibar nchini China, ataja fursa ikiwemo bandari
2023-06-29 21:17:42| cri

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Han Zheng, huku akinadi fursa zilizopo visiwani humo.

Katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika jana Juni 28 2023, viongozi hao wamepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya Tanzania na China. Rais Mwinyi ameipongeza Serikali ya China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya maendeleo kwa miaka 59 sasa tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Dk Mwinyi amebainisha uamuzi wa hivi karibuni wa viongozi wakuu wa nchi hizi mbili Samia Suluhu Hassan na Xi Jinping wa kufungua zaidi njia kuu za uhusiano ambazo zimesaidia kuimarisha uhusiano huo. Aidha Rais Mwinyi amemweleza Makamu huyo wa Rais wa China sera kuu ya Zanzibar ya uchumi na kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kusaidia katika uwekezaji.

Kwa upande wake makamu wa rais Han Zheng, alimhakikishia Dk Mwinyi kwamba nchi yake imejizatiti kuiunga mkono Zanzibar kufikia hatua kubwa ya maendeleo ambapo amesema kwa sasa Serikali yao inawahimiza watalii wengi wa China kuitembelea Zanzibar.

Leo Alhamisi Juni 29, 2023 Rais Mwinyi akiendelea na ziara nchini China anatazamiwa kuhudhuria maonesho makubwa ya tatu ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika katika mji wa Changsha na baadaye atakuwa na mkutano maalumu katika sekta ya afya.