Bibi Peng Liyuan ahutubia Baraza la Wanawake la China na Afrika kwa njia ya video
2023-06-29 16:01:35| CRI

Mke wa Rais wa China Bibi Peng Liyuan ambaye ni mjumbe maalumu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO anayeshughulikia kuhimiza elimu kwa wanawake na watoto wa kike, amehutubia Baraza la Wanawake la China na Afrika kwa njia ya video.

Kwenye hotuba yake, Bibi Peng Liyuan amesema, China na Afrika zote zinatilia maanani kuhimiza maendeleo ya wanawake. China siku zote inajitahidi kukamilisha mfumo wa sheria unaolinda haki za wanawake, kuinua kiwango cha elimu kwa wanawake, kuwaunga mkono kujihusisha na ujasiriamali na uvumbuzi, na kukamilisha huduma kwa wanawake na watoto, ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo ya wanawake katika pande zote. Nchi za Afrika pia zinajitahidi kuboresha mazingira ya kazi na maisha kwa wanawake, kuwaondoa kwenye umaskini, kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye usimamizi wa nchi na jamii, na juhudi hizo zimezaa matunda. Bibi Peng amesema kuwa China na Afrika zenye nia na dhamira ya pamoja siku zote zinasonga mbele bega kwa bega kwenye safari ya kuhimiza maendeleo ya wanawake.

Baraza la Wanawake la China na Afrika lililoandaliwa na Shirikisho la Wanawake la China kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Hunan, limefunguliwa leo Juni 29 mjini Changsha.