China na Tanzania zafanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa teknolojia ya habari
2023-06-29 22:17:02| cri

Tanzania imethibitisha kuwa imeanza mazungumzo na Shirika la Sayansi na Teknolojia la Anga la China (CASC) ili kuimarisha teknolojia ya habari.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amefanya kikao na shirika hilo jana Jumatano akiwa na Katibu Mkuu wake, Maafisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC) na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC.

CASC ni mkandarasi mkuu wa anga za juu wa China ambaye amefanya majaribio kadhaa yenye mafanikio ya kupeleka chombo cha anga za juu kama sehemu ya mipango ya kukusanya sampuli za asteroid na kuzileta salama duniani.

Bw. Nape alisema kwa ufupi baada ya mkutano kuwa pande hizo mbili zinalenga kuimarisha ushirikiano katika teknolojia ya anga ya juu na ulinzi wa taarifa binafsi.

“Hii ni sehemu ya mikakati ya serikali katika kujenga na kukuza uchumi wa kidijitali ambao utatoa maisha bora kwa Watanzania kupitia TEHAMA,” amesema.

Hatua hiyo mpya imekuja kufuatia uamuzi wa China wa kupanua sera yake ya diplomasia ya anga ya juu kwa kuzikaribisha nchi mbalimbali hasa nchi za Afrika kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uchunguzi wa anga, kuboresha sayansi na kuzalisha wanaanga wengi.