Waziri Mkuu wa China afanya mazungumzo na wenzake wa New Zealand na Mongolia
2023-06-29 08:38:03| cri

Waziri Mkuu wa China Bw. Li Qiang amekutana kwa nyakati tofauti na Waziri Mkuu wa New Zealand Chris Hipkins na wa Mongolia, Luvsannamsrai Oyun-Erdene ambao walikuwa katika ziara rasmi nchini China.

Katika mazungumzo yake na Bw. Hipkins, Bw. Li amesema China inapenda kushirikiana na New Zealand kutumia fursa mpya zinazoletwa na maendeleo yake, na kutetea kwa pamoja biashara huria, kuunga mkono ushirikiano wa kikanda katika eneo la Asia-Pasifiki, na kupanua "nafasi mpya" ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.

Bw. Hipkins amesema, New Zealand inafuata kithabiti sera ya China moja na inapenda kuzidisha ushirikiano na China katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, biashara, sayansi na teknolojia na elimu.

Alipokutana na Bw. Oyun-Erdene, Bw. Li alisema, China inapenda kushirikiana na Mongolia kuendeleza uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi hizo mbili, kuzidisha uaminifu wa kisiasa na ushirikiano wa kunufaishana, na kuharakisha ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Bw. Oyun-Erdene alisema, Mongolia iko tayari kuimarisha sera ya maendeleo ya muda mrefu ya "Ruwaza ya Mwaka 2050" ya Mongolia na Pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja.