Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) jana jumatano limetoa wito wa msaada wa dharura ili kujiandaa kukabiliana na mafuriko zaidi yanayotarajiwa kutokea baadaye mwaka huu kutokana na mfumo wa hali ya hewa wa El Nino.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu mwitikio wa ukame katika Pembe ya Afrika iliyotolewa jana jumatano, Shirika hilo limesema, kuanzia mwezi Januari mwaka jana, limeongeza mwitikio wake kuhusu ukame katika eneo hilo, na kutoa msaada muhimu kwa zaidi ya watu milioni 4.3 nchini Sudan na Ethiopia.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, mpaka kufikia mwezi Mei mwaka huu, sehemu nyingi zilizoathiriwa na ulame katika kanda ya Pembe ya Afrika zilikuwa katika mwelekeo sahihi wa kupokea kiasi kikubwa cha mvua, ingawa baadhi ya maeneo yameendelea kushuhudia ukame, hususan katikati ya Somalia.
Hata hivyo Shirika hilo limeonya kuwa, mvua zimesababisha mafuriko ya ghafla na kuathiri watu zaidi ya 900,000 katika kanda hiyo, kuhatarisha zaidi mlipuko wa magonjwa yanayosababishwa na uchafu wa maji, hususan kati ya makundi yaliyo dhaifu kutokana na utapiamlo.