Rwanda yaahidi kushikilia ahadi yake ya makubaliano ya uhamiaji
2023-06-30 08:41:35| CRI

Serikali ya Rwanda imesema itashikilia kikamilifu ahadi yake ya makubaliano ya wahamiaji na Uingereza, ikiwa ni kujibu uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufani ya Uingereza unaodai kuwa mpango wa kuhamisha watu wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda sio halali kisheria.

Uingereza na Rwanda zilifikia makubaliano hayo mwezi April mwaka jana, ambao unaelekeza kuwa wahamiaji haramu na watu wanaotafuta hifadhi watapelekwa nchini Rwanda na madai yao kusikilizwa nchini humo.

Jana, Mahakama ya Rufani ya Uingereza ilibadili uamuzi uliotolewa mwezi Desemba na Mahakama ya Juu nchini humo, ambao ulisema Rwanda ni nchi salama ya tatu kwa watu wanaotafuta hifadhi na wakimbizi.

Hata hivyo, katika taarifa yake, serikali ya Rwanda imesema haikubaliani na uamuzi huo, na haikubaliani na kauli kwamba Rwanda sio nchi salama kwa wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi.