Wakurugenzi wakuu wa barani Afrika wamesema, ukuaji wa uchumi wa kidijitali barani humo umeendana na kuibuka kwa matishio dhidi ya usalama wa mtandao yanayolenga makampuni, ikiwemo udukuzi na kuvuja kwa taarifa binafsi.
Wakizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti ya “Maendeleo ya Usalama wa Mtandao barani Afrika mwaka 2022”, wakurugenzi hao wamezitaka kampuni katika bara hilo kuimarisha uwekezaji katika ulinzi wa mtandao na kukwepa kuingiliwa na wahalifu katika miundombinu yao ya kidijitali.
Ripoti hiyo imesema zaidi ya nusu ya kampuni kubwa katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Zambia ni wahanga wa mashambulizi ya mtandao yaliyofanyika mwaka jana.
Pia ripoti hiyo imesema, uwekezaji mdogo katika ulinzi wa mtandao, pengo la ujuzi, sera zisizofungamana na mazingira ya kanuni, na ukosefu wa data zinazofika kwa wakati, vimedhoofisha mwitikio kwa matishio dhidi ya mtandao katika kampuni za barani Afrika.