Zaidi ya watu milioni 2.6 nchini Sudan wamekimbia makazi yao tangu vita ilipoanza nchini humo katikati ya mwezi April mwaka huu, huku watu wengine 560,000 wakikimbilia katika nchi jirani za Misri, Chad na Sudan Kusini.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema, zaidi ya watu milioni 2.1 wamekuwa wakimbizi wa ndani tangu April 15, wakiwemo watu milioni 1.4 walioukimbia mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
OCHA imesema mashirika ya kibinadamu yamewafikia watu zaidi ya milioni 2.8 nchini humo kwa kuwapelekea chakula, lishe, huduma za afya, maji na ulinzi. Hata hivyo, wenzi wa kibinadamu wanasema wanakwama katika kazi zao kutokana na hali ya kutokuwa na usalama na urasimu, pamoja na ukosefu wa visa kwa wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali.