Watoto huzaliwa wakiwa hawana hatia. Wanataka kupendwa, kujifunza, na baadaye wakiwa wakubwa wawe mchango mkubwa katika jamii. Lakini kuna baadhi ya wazazi huwa hawathamini ukweli huu na matokeo yake huwa wanakosa muda mzuri na wa thamani zaidi katika maisha ya watoto wao. Tukizungumzia suala la utumikishaji ama kazi za kulazimishwa katika sehemu nyingi duniani, basi watoto wanaonekana kuwa ni wahanga wakubwa. Hivyo hivi karibuni yaani tarehe 12 mwezi Juni ni siku maalumu iliyotengwa duniani kwa ajili ya kupinga ajira kwa Watoto duniani.
Mbali na tarehe hiyo kuwa maalumu kwa ajili ya kupinga ajira kwa watoto, pia barani Afrika wametenga kila ifikapo tarehe 16 ya mwezi wa 6 pia kuwa ni siku ya kimataifa ya mtoto wa Afrika. Na kwa mada huu kauli mbiu yake ni elimu kwa mtoto wa Afrika kwa ajili ya maisha mema ya baadae. Hivyo katika kipindi hiki cha Ukumbi wa wanawake leo tutaangalia suala la ajira kwa watoto na pia kuiangalia siku ya mtoto wa Afrika.