Katika miaka ya karibuni kumekuwa na aina Fulani ya maisha tunaweza kusema, ambapo watu wanene wamekuwa wakikosolewa na kusemwa vibaya katika mitandao ya kijamii na hata uso kwa uso. Kauli kama vile ‘bonge’, ‘tembo mtoto’, ‘tipwatipwa’ huwa zinatumika sana kuwaambia watu kuwa wamezidi unene. Hilo linapotokea, tena hususan kwa wanawake, mara nyingi wanachukua hatua kali ili kupunguza uzito, bila kujali athari za hatua hizo kiafya. Kuna diets mbalimbali zinazosemwa kuwa zinasaidia kupunguza uzito haraka, na wengi wanazikimbilia hizo ili tu waweze kwenda sawa na mtazamo wa jamii kuhusu maumbile.
Hili ni jambo ambalo kimsingi linapaswa kutazamwa kwa umakini wa kipekee. Ni kweli kwamba unene uliopitiliza ni hatari kwa afya, lakini pia kuwa na uzito mdogo uliopitiliza pia ni hatari kwa afya. Kwa wanawake, suala hili la unene na wembamba ni kama utambulisho wa mtu. Tunajua kuwa kila mtu ana maumbile yake, hivyo mtu anapochukua hatua ya kumsema mtu mwingine ama kumuita kwa majina ambayo yanadhalilisha, hiyo inakuwa ni kama njia ya kumfanya mtu anayesemwa kutafuta suluhisho ili aonekane naye anapendeza. Katika kipindi chetu che leo cha Ukumbi wa Wanawake, tutaangalia suala hili la kupunguza uzito kupita kiasi, na athari zake kwa afya, hususan kwa mwanamke.