Jitihada mpya zalenga kusuluhisha mjadala wa zamani kuhusu ni mto upi mrefu zaidi, Amazon au Nile?
2023-07-01 20:18:23| cri

Ni mto gani mrefu zaidi duniani, Nile au Amazon? Swali hilo limezua mjadala mkali kwa miaka mingi. Sasa, msafara katika msitu wa Amerika Kusini unalenga kutoa jibu la swali hilo.

Kwa kutumia boti zinazoendeshwa kwa nishati ya jua na nguvu ya miguu, timu ya kimataifa ya wavumbuzi inapanga kuondoka Aprili 2024 kwenye chanzo cha Amazon katika milima ya Andes ya Peru, kisha kusafiri karibu kilomita 7,000 (maili 4,350) nchini Colombia na Brazil, hadi mdomo wa mto kwenye Atlantiki. Mratibu wa mradi huo ambaye ni mgunduzi wa Brazil Yuri Sanada, alisema lengo kuu ni kuchora ramani ya mto na kuweka kumbukumbu za viumbe hai vya mfumo wa ikolojia unaozunguka mto huo.

Amazon, umetambuliwa kwa muda mrefu kama mto mkubwa zaidi duniani kwa ujazo, ukitoa maji zaidi ya Nile, Yangtze na Mississippi kwa pamoja. Lakini kuna mzozo wa kijiografia wa miongo kadhaa juu ya kama Mto Nile au Amazon ndio mrefu, hata hivyo kitabu cha kumbukumbu za rikodi za dunia ‘Guinness World Records’ kimeutaja mto wa Afrika, Nile ndio mrefu zaidi.