China imeahidi kuimarisha ushirikiano wake na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kujenga uwezo, biashara, maendeleo ya miundombinu na nyanja nyinginezo.
Balozi wa China nchini Tanzania na EAC, Chen Mingjian, alisema katika Makao Makuu ya EAC mjini Arusha kuwa China ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani ina matumaini makubwa ya kukuza uchumi sio tu katika EAC bali katika bara zima la Afrika. Akikabidhi magari manane, mabasi matatu na pick-up tano kwa EAC Balozi Mingjian amebainisha kuwa China inathamini sana mchango mkubwa unaotolewa na EAC katika kudumisha amani na utulivu wa kikanda, kuboresha miundombinu ya kikanda, kupigana kwa pamoja dhidi ya UVIKO-19, kukuza mafungamano ya kiuchumi ya kikanda na kufufua uchumi wa nchi za kanda hiyo.
Mjumbe huyo alisema msaada huo wa dola za Marekani 400,000 wa magari kutoka serikali ya China utasaidia EAC katika kuboresha uwezo wake wa kuandaa na kuratibu mikutano na matukio katika kanda nzima.
Balozi Mingjian amesema China pia imetuma mafundi na vipuri vya magari mbalimbali ili kusaidia katika matengenezo na uendeshaji wa magari hayo.