Makampuni 50 China kushiriki sabasaba
2023-07-03 22:52:13| cri

Wafanyabiashara wa kampuni zaidi ya 50 nchini China, wamewasili Tanzania jana Jumapili Julai 2, 2023 kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya kimataifa ya Sabasaba, wakiahidi kuonyesha bidhaa mbalimbali katika maonyesho hayo ikiwemo vifaa vya kielektroniki. Vifaa hivyo ni pamoja na miradi, kompyuta, simu za mkononi na teknolojia mbalimbali mpya ambazo zimebuniwa na zimeshaanza kutumika.

Akizungumza mara baada ya mapokezi hayo, Kaimu Mkurugenzi Uwekezaji Biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Fortunatus Mhambe amesema ujumbe huo ni kati ya ushirikiano kati ya Tanzania na China na kwamba licha ya kuonyesha bidhaa pia wanakuja kwa ajili ya Uwekezaji. Meneja wa Kituo cha biashara cha Afrika Mashariki, Wang Xiangyu amesema kupitia maonyesho hayo Watapata fursa mbalimbali hivyo ni muhimu kuwatembelea.

Jumla ya nchi 14 zimethibitisha kushiriki maonyesho hayo yanayofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 14 mwaka huu, ambapo kampuni 112 kutoka nje ya nchi na 1,188 za ndani zinashiriki.