Wanafunzi wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Ghana wameanza tena maadhimisho ya kila mwaka ya wiki ya lugha ya kichina baada ya kusimama kwa miaka mitatu kutokana na janga la COVID-19.
Wakati wa hafla ya ufunguzi mwenyekiti wa jumuiya ya wanafunzi wa lugha ya kichina katika Chuo Kikuu hicho Bw. Herbert Danquah, alisema maadhimisho hayo, ambayo sasa yametimiza miaka 14, yataendelea kuchangia kuimarisha uhusiano wa kitamaduni kati ya China na Ghana. Amesema shughuli za wiki ya lugha ya Kichina zitawaleta pamoja wanafunzi wa zamani wa lugha ya Kichina, wataalam wa uhusiano kati ya China na Afrika na watu binafsi ambao wamefanya kazi na wachina kwenye mambo ya uhusiano kati ya China na Ghana.
Mkuu wa zamani wa chuo hicho Prince Akantogdaam, alisema anafurahi kuwa sherehe hizo zinarejea tena katika chuo kikuu, na kuongeza kuwa wanafunzi wanaopenda kujifunza lugha ya Kichina wameongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni.