Wakati wa maonyesho ya 3 ya kimataifa ya Uchumi na biashara kati ya China na Afrika yaliyofanyika kati ya Juni 29 na Julai 2 mjini Changsha China, wataalamu wa uchumi walipitia takwimu za thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili, ambayo imeonekana kuongezeka kutoka Yuan Bilioni 100 kwa mwaka 2000, hadi kufikia Yuan Trilioni 1.8 (Dola za Marekani bilioni 260) za mwaka 2022. Licha ya kuwa takwimu hizi zinaridhisha, wataalamu wanaona kutokana na kuwa kuna maeneo mengi ya ushirikiano ambayo bado hayajatumiwa ipasavyo, thamani hiyo ingeweza kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.
Maonyesho hayo yamefanyika chini ya kauli mbiu ya “maendeleo ya pamoja kwa mustakbali wa pamoja”, kauli ambayo inaakisi azma ya China ya kutoziacha nyuma nchi Afrika wakati yenyewe ikiendelea kujiendeleza. Akiongea wakati wa ufunguzi wa maonyesho hayo, makamu wa Rais wa China Bw. Han Zheng alikumbusha ahadi ya China, kuwa itaendelea kuwa imara katika kuziunga mkono nchi za Afrika kwenye kujitafutia njia ya maendeleo ya kujitegemea na inayolingana na mazingira ya nchi za Afrika. Zaidi ya hapo alikumbusha tena kuwa China itaendelea kuhimiza ushirikiano kati yake na nchi za Afrika chini ya pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na kuhimiza maendeleo ya viwanda na miundo mbinu ya kuziunganisha nchi za Afrika.
Alichokiongea makamu wa Rais Bw. Han Zheng, kimsingi kimeanza kuonekana barani Afrika, na maonyesho yenyewe ya Changsha pia ni ushahidi wa alichokisema. Tukiangalia kwa undani tunaweza kuona kuwa changamoto kubwa ya uchumi wa nchi za Afrika ni kuwa unaendeshwa kwa nadharia za kimagharibi katika mazingira yasiyokuwa ya kimagharibi. Matokeo yake ni kuwa nchi nyingi za Afrika zimejikuta zimekwama bila kuwa na maendeleo makubwa. Lakini tangu nchi za Afrika zilipoanza kujitafutia njia mbadala za kujiendeleza, matumaini yanaonekana na kumekuwa na ongezeko la uchumi. Ndio maana Bw. Han Zheng amesema China itaendelea kuziunga mkono nchi za Afrika katika njia hiyo.
Wengi pia tunaweza kukumbuka kuwa changamoto kubwa ya maendeleo ya Afrika ni kudumaa kwa sekta ya viwanda, ambayo kimsingi imebaki kama ilivyokuwa wakati walipoondoka wakoloni. Katika baadhi ya nchi inaonekana kuwa hata kilichoachwa na wakoloni hakipo tena. Hali kama hiyo pia imeonekana kwenye miundo mbinu mingi ya nchi za Afrika. Nchi za Afrika zimeanza kuchukua hatua kurekebisha dosari hizo.
Tukiangalia maonyesho ya Changsha ya mwaka huu, pia tunaweza kuona matunda ya ushirikiano kwenye sekta za viwanda na miundo mbinu kati ya China na nchi za Afrika. Wajasiriamali wengi waliokuja kutoka Afrika, wamesema bidhaa nyingi walizokuja kuonyesha na kuuza zimetengenezwa kwa zana zilizotoka China, na baadhi walisema vifungashio vya bidhaa zao vimetengenezwa China, na wengine walisema bidhaa zao zilizosafirishwa kutoka mashambani hadi bandarini, zilipita kwenye baadhi ya barabara zilizotengenezwa na makampuni ya China.
Kama kauli mbiu ya maonyesho haya ilivyosema, “maendeleo ya pamoja kwa mustakbali wa pamoja”, ni kweli maendeleo ya China yamekuwa neema kwa nchi mbalimbali za Afrika. Kwa sasa watu wa Afrika wamekuwa na uwezo zaidi wa kuzalisha bidhaa kutokana na kupata zana zenye bei nafuu kutoka China. Na kutokana na China kufungua soko lake kwa nchi za Afrika, kilio cha muda mrefu kuhusu kukosa masoko sasa kinazidi kupungua, na thamani ya biashara kati ya pande mbili inazidi kuongezeka.