Sekta ya kuchakata, kusindika na kufunga bidhaa itatoa mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania
2023-07-04 13:56:24| CRI

Kwenye maonyesho ya tatu ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika yaliyofanyika hivi karibuni katika mji wa Changsha mkoani Hunan, bidhaa nyingi kutoka Afrika zilioneshwa na kuvutia wateja wengi wa China. Licha ya kuwa waonyesha bidhaa hizo walipata wateja wengi na kuuza bidhaa zao, moja ya dosari zilizoonekana ni kuwa baadhi ya bidhaa ziliendelea kuwa katika hali ghafi bila kuongezwa thamani vya kutosha, na hivyo kutopata faidi kubwa.

 

Mwamko wa wateja wa China kuchangamkia bidhaa za Afrika umekuwa wazi sana, iwe ni korosho, ufuta, asali na hata maharage. Lakini moja ya changamoto kubwa iliyoonekana kwenye bidhaa hizo ni kuwa uchakataji, usindikaji na ufungaji wa bidhaa kutoka Afrika zinazouzwa katika masoko ya China bado una changamoto kubwa. Wachina ni watu wanaochangamkia sana bidhaa kutoka Afrika, kwani wanajua kuwa bidhaa za kilimo na chakula zinazozalishwa katika maeneo ya kitropiki zina ladha ya kipekee na lishe bora ikilinganishwa na bidhaa za kilimo zinazozalishwa katika njia zisozo za kiasili.

 

Tukiangalia zao la Korosho, wachina ni watumiaji wakubwa wa zao la Korosho, na wengi wanajua kuwa korosho tamu wanayotumia inatoka katika nchi za kusini mwa Asia. Lakini ukweli ni kwamba korosho hiyo ni ile inayotoka katika nchi za Afrika, na kwenda kuongezwa thamani katika nchi za Asia ya Kusini na kuletwa kuuzwa katika soko la China. Kwa sasa baadhi ya nchi zimeanza kuchukua hatua ya kuchakata korosho, lakini bado kuna udhaifu kwenye kuongeza thamani na hata kufungasha.

 

Bidhaa nyingine ambayo inaweza kuongezwa thamani na kuwa na faida kubwa ni maharage ya soya. Kwa sasa nchi zinazouza maharage ya soya nchini China, bado zinauzwa punje za maharage ya soya na sio bidhaa zinazotokana na punje hizo. Pamoja na kuwa wachina ni waagizaji wakubwa wa maharage ya soya, ukweli ni kuwa hawatumii maharage hayo kama chakula, bali wanatumia maharage hayo kwa kutengeneza kinywaji chenye lishe ya protini kinachoitwa doujiang, au kwa kusagwa na kugandishwa kuwa jeli yaani tofu na kutumiwa kama kitoweo au kuchanganya na chakula kingine.

 

Kama wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika wangekuwa wanasafirisha doujiang na tofu kuja kwenye soko la China, basi faida ambayo wangepata ingekuwa ni kubwa sana. Kwa sasa ni Afrika Kusini tu ndio imeonekana kupiga hatua sana kwenye uchakataji, usindikaji na hata ufungaji wa bidhaa zake. Mfano mzuri ni mvinyo wa Afrika Kusini, ambao sasa umeingia kwenye soko la China na kuwa na nguvu kubwa ya ushindani hata kuliko mvinyo kutoka katika nchi za Ulaya.

 

Jambo la kufurahisha ni kuwa China imepiga hatua katika maeneo hayo yote, kwani minyororo yake ya uzalishaji wa bidhaa imekamilika kutoka hatua ya kuvuna hadi kusindika, kufungasha na kumfikishia mteja. Hili linaweza kuwa ni eneo zuri sana la ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika. Kwa sasa baadhi ya makampuni ya China yameanza kuingia kwenye maeneo hayo, lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazotakiwa kuondolewa kabla ya kufikia hatua ya kuongeza thamani bidhaa za kilimo kabla ya kuzisafirisha.

 

Fursa ya soko la bidhaa za kilimo kwa nchi za Afrika nchini China inaonekana kuwa endelevu, kwa sasa ni jukumu la wafanyabiashara wa pande mbili kuangalia ni njia ipi inaweza kuleta manufaa zaidi kwa wao wenyewe, kwa wateja wao na hata kwa nchi zao. Bila shaka kuchakata bidhaa za kilimo, kuzisindika na kuziweka katika vifungashio vizuri, ndio njia sahihi ya kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuzifikisha kwenye soko la China kwa faida kubwa zaidi.