Rais Xi Jinping wa China jana Julai 3 alituma barua ya pongezi kwa Mazungumzo ya tatu ya Kufundishana kati ya Staarabu na Mkutano wa Kwanza wa Wataalamu wa Mambo ya China Duniani uliofunguliwa siku hiyo hapa Beijing.
Kwenye barua yake, Rais Xi amebainisha kuwa kwenye historia ndefu ya binadamu, mataifa mbalimbali duniani yameanzisha staarabu zenye umaalumu na alama zao. Kuwasiliana kwa usawa na kufundishana kati ya staarabu tofauti, kutatoa mwongozo imara wa kiroho kwa binadamu kutatua changamoto za zama zao na kutimiza maendeleo ya pamoja.
Rais Xi amesisitiza kuwa China inapenda kushirikiana na pande mbalimbali katika kuenzi na kurithisha maadili ya pamoja ya binadamu wote ambayo ni amani, maendeleo, haki, demokrasia na uhuru, kutekeleza Pendekezo la Staarabu Duniani na kusukuma mbele kwa pamoja maendeleo ya staarabu za binadamu. Rais Xi pia ameeleza matumaini yake kuwa wataalamu wa mambo ya China kutoka nchi mbalimbali watakuwa mabalozi wa kuunganisha staarabu za China na nchi za nje, na kufanya juhudi zaidi kwa ajili ya kuzidisha maelewano, urafiki na ushirikiano kati ya China na nchi za nje.