Sudan Kusini yatangaza mlipuko wa surua miongoni mwa watu waliorejea katika jimbo la Unity
2023-07-04 09:26:54| CRI

Mamlaka za afya za Sudan Kusini katika kaunti ya Rubkona jimboni Unity zimetangaza mlipuko wa surua miongoni mwa watu waliorejea makwao baada ya kukimbia mgogoro nchini Sudan.

Mkurugenzi wa afya kaunti ya Rubkona Bw. Jal Kuol Malow amesema sasa kuna watu 86 waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huo katika eneo hilo, wengi wao wakiwa ni watoto wenye umri wa miaka minne hadi sita, ambao hawakupewa chanjo ya surua walipokuwa nchini Sudan.

Ameongeza kuwa wizara ya afya ya Sudan Kusini na washirika wake wa kibinadamu, wameanzisha kampeni ya kutoa chanjo kwa watu waliorudi huko Rotriah Payam, na wiki hii kampeni kama hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika eneo la Rubkona na kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bentiu.