Mwanariadha wa mbio za marathon wa Kenya Ekiru apigwa marufuku kwa muda kwa kutumia dawa za kusisimua misuli
2023-07-04 20:04:31| cri

Kitengo cha Uadilifu cha Riadha (AIU) kimesema Jumatatu kwamba mwanariadha wa Kenya Titus Ekiru, ambaye ni wa sita kwa kasi zaidi katika historia ya mbio za marathon, ana uwezekano wa kufungiwa miaka 10 baada ya kusimamishwa kwa muda kwa kutumia dawa za kusisimua misuli.

Ekiru ameshinda marathon mbili ikiwa ni pamoja na ushindi wa Milan alioupata Mei 2021 kwa kutumia kasi ya kipekee ya muda wa saa 2 dakika 2min 57sec.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alipimwa na kukutwa na triamcinolone acetonide na glukokotikoidi mwilini, baada ya kushinda mbio za Milan, lakini hakushtakiwa mara moja baada ya uchunguzi wa awali kuthibitisha maelezo yake ya kwamba majibu hayo ya vipimo yalitokana na matibabu halali. Mwanariadha huyo alipimwa na kukutwa na pethidine baada ya kushinda huko Abu Dhabi mwezi Novemba, 2021, na alidai kuwa majibu hayo yalitokana na matibabu halali, na tokea wakati huo hajakimbia tena.

"Kufuatia uchunguzi wa awali kuhusu suala hilo, na kutokana na kuibuka kwa mtindo wa matumizi ya acetonide ya triamcinolone miongoni mwa wanariadha wa Kenya, AIU ilifungua upya uchunguzi wa tukio la kwanza la Ekiru," AIU ilisema.

Mwezi uliopita Ekiru alisimamishwa kwa muda, akisubiri matokeo ya uchunguzi wa pande zote mbili ambao ulijumuisha ushirikiano muhimu na Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya la Kenya (ADAK) na mamlaka nyingine za Kenya.

Hilo lilipelekea AIU kukataa maelezo ya Ekiru, ikimshtaki kwa makosa mawili ya dawa za kuongeza nguvu mwilini, kisha kudai kwamba Mkenya huyo "ana kesi za kujibu kwa kuvuruga michakato ya usimamizi wa matokeo kwa kuwasilisha maelezo ya kimatibabu na nyaraka za uongo kwa AIU kwa vipimo vyote viwili".

AIU ilisema hii ina maana kwamba mwanariadha huyo wa mbio za marathoni anakabiliwa na marufuku ya miaka 10.