Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amesema maadandalizi ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani yamekamilika.
Amesema maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika Julai 7, Zanzibar yataambatana na shamra shamra mbalimbali zikiwemo muziki wa taarabu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Lengo la kuadhimisha Siku ya Kiswahili ni kuieleza dunia kuwa chimbuko la Kiswahili ni Tanzania,” alisema waziri.
Maadhimisho hayo yalianza rasmi mwaka 2022 baada ya kutangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021. Kwa upande wake katibu mkuu wizara ya utamaduni, sanaa na michezo Saidi Yakubu amesema tamasha hilo litahudhuriwa na watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ujerumani, Ghana, Kenya, Visiwa vya Comoro na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao huko nchini Tanzania.