Rais Xi atoa wito wa umoja na uratibu katika Mkutano wa Kilele wa SCO
2023-07-05 08:44:46| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) inapaswa kujitokeza kuitikia wito wa zama, kukumbuka jukumu lake la asili, na kudumisha umoja na uratibu ili kuleta uhakika na ushawishi chanya kwa ajili ya amani na maendeleo ya dunia.

Rais ameyasema hayo wakati akihutubia kwa njia ya video mkutano wa 23 wa Baraza la Wakuu wa Nchi Wanachama wa SCO. Amesema nchi wanachama zinapaswa kujiweka katika mwelekeo sahihi na kuimarisha hali ya kushikamana na kuaminiana; kuongeza mawasiliano na uratibu wa kimkakati na kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo, na pia zinatakiwa kukumbuka maslahi ya jumla na ya muda mrefu ya kikanda, na kudumisha amani ya kikanda na kulinda usalama wa pamoja.

Rais Xi pia ametoa wito wa kuongeza ushirikiano wa SCO kwenye nyanja ya usalama, na kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi, ufarakanishaji, itikadi kali, magendo ya dawa za kulevya, na uhalifu wa kupangwa wa kuvuka mipaka na kwenye mtandao, na pia kupanua ushirikiano kwenye maeneo ya usalama usio wa jadi, ikiwemo ya dijitali, baolojia na kwenye anga ya juu.