Idara ya takwimu ya Kenya (KNBS) imesema ongezeko la uchumi wa Kenya limedorora hadi kufikia asilimia 5.3 katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kutoka asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka jana, ukiathiriwa na kupungua kwa shughuli za sekta za uzalishaji viwandani, ujenzi na uchukuzi.
KNBS imesema katika ripoti yake kuwa sekta ya kilimo ilikuwa na ongezeko na ilisaidia kupunguza kasi ya kushuka kwa ukuaji wa uchumi. Ongezeko hilo la asilimia 5.3 lilitokana kwa kiasi kikubwa na kurejea kwa shughuli za kilimo, ambazo zilikua kwa asilimia 5.8, kutokana na mvua za kutosha zilizonyesha katika kipindi hicho.
Mwaka jana katika kipindi kama hicho sekta hii ilikuwa na ongezeko la asilimia 1.7 wakati Kenya ilipokuywa inasumbuliwa na ukame. Sekta nyingine zilizorekodi ukuaji katika robo ya kwanza ni pamoja na huduma za malazi na chakula (asilimia 21.5) Tehama (asilimia 8.7), fedha na bima( asilimia 5.8), na biashara ya jumla na rejareja (asilimia 5.7).