Tanzania kuwa kituo kikubwa cha biashara Afrika Mashariki na Kati
2023-07-05 21:42:46| cri

Mradi mkubwa wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki ‘East Africa Commercial and Logistics Centre’ (EACLC) unaojengwa Ubungo unatarajiwa kuwa kiunganishi kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na ndio wadhamini wakuu wa Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba’.

Hayo yamesemwa jana Julai 4, 2023 na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba’ .

Amesema, mradi huo ambao una thamani ya dola za Kimarekani milioni 81.827 utaifungua Tanzania kibiashara na kukuza uchumi kutokana na biashara zitakazokuwa zikifanyika na kukuza mahusiano ya Kimataifa kwa kuwa na muingiliano wa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.

Kituo hicho kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi 15,000 na kuhamasisha maendeleo ya sekta mbali mbali ambazo nazo zitazalisha ajira zisizo za moja kwa moja 50,000 hivyo kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wa Tanzania.

Mradi huo unatarajiwa kuwa na maduka 2060 yenye ukubwa wa jumla ya mita za mraba 75,000 ambapo eneo hilo litakuwa na huduma zote za kibiashara ikiwemo mabenki na huduma za ufungishaji na usafirishaji.

Pia, mradi huo ukikamilika mapato ya jumla kwa mwaka yanatarajiwa kufikia zaidi ya USD Milioni 500 hivyo kusaidia katika ukuaji wa pato la Taifa la Tanzania na kuongeza mapato ya kodi.