Maonyesho ya Tatu ya Biashara ya China na Afrika yamemalizika hivi karibuni hapa China, ambapo bidhaa mbalimbali kutoka nchi za Afrika ikiwemo kahawa kutoka Ethiopia, maua kutoka Kenya, na bidhaa nyingine nyingi zimeendelea kupata umaarufu kwenye soko la China.
Maonesho hayo yalianza mjini Changsha Alhamis iliyopita na kuwaletea wateja wa China bidhaa za ubora wa juu na bei nafuu, na kupata matokeo ya kunufaishana. Kwa wazalishaji wa Afrika na wafanyabiashara wanaotafuta masoko mapya, maonyesho hayo ni fursa adimu sana. Washiriki 1,500 katika maonyesho wametoa taswira kuwa maonyesho ya mwaka huu yatazisaidia China na Afrika kuanzisha ushirikiano mpya na kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa pande mbili.
Kati ya bidhaa za kilimo zilizoonyeshwa, bidhaa ya parachichi ni mfano unaoonyesha maendeleo ya biashara kati ya China na Afrika. Kuanzia mwezi Julai mwaka jana, Kenya imesafirisha zaidi ya tani 3,000 za parachichi nchini China, na kuongeza kipato kwa wakulima zaidi ya 3,200 wa zao hilo. Maofisa wa kilimo nchini Kenya wanatarajia kuwa, mauzo ya parachichi nchini China yataongezeka na kufikia tani 100,000 katika miaka ijayo.
Wakati wa Mkutano wa ngazi ya Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2021, China ilitangaza kuanzisha ‘njia ya kijani’ kwa bidhaa za kilimo kutoka nchi za Afrika kuingia nchini China, na tangu wakati huo, nchi nyingi za Afrika zimepata kibali cha kuingiza bidhaa zao za kilimo, kama vile ufuta kutoka Tanzania katika soko la China.
Katika maonesho ya Changsha, kwa mara ya kwanza Wachina walipata fursa ya kuonja dagaa wa maji chumvi kutoka nchini Kenya. Dagaa hao walikaushwa na kufungashwa katika kampuni ya Ukanda wa Uzalishaji wa Chakula wa Huawen, ambayo iko katika Kaunti ya Kwale nchini Kenya.
Katibu wa Wizara ya Madini, Uchumi wa Kijani na Masuala ya Baharini nchini Kenya, Salim Mvurya amesema, shehena ya kwanza ya dagaa kutoka kwa wavuvi wa Kenya kupelekwa kwenye soko la China ni hatua ya kihistoria kwa nchi hiyo.
Kwa miaka mingi, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika umeshuhudia maendeleo ya utulivu, na utekelezaji wa miradi mingi kupitia majukwaa kama Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), na Maonyesho ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika, na ushirikiano kati ya pande hizo mbili umepata matokeo mazuri ya kunufaishana.
Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya China, nchi hiyo imeendelea kuwa mwezi mkubwa wa biashara wa Afrika kwa miaka 14 mfululizo. Pande hizo mbili kwa pamoja zimejenga zaidi ya kilomita 10,000 za reli ambazo zinatumika, karibu kilomita 100,000 za barabara kuu, na miundombinu mbalimbali muhimu ikiwemo viwanja vya ndege, bandari, madaraja na vituo vya nishati.
Katika miaka ya karibuni, ushirikiano kati ya China na Afrika umepanuka zaidi kutoka kilimo, miundombinu, na uzalishaji, na kuingia kwenye sekta mpya kama uchumi wa kijani, afya, fedha na uvumbuzi wa kidijitali.
Balozi wa Afrika Kusini nchini China, Siyabonga Cyprian Cwele anasema, biashara inayoendelea kukua ni hali ya kunufiashana, na ukuaji wa uhusiano wa biashara ya pande mbili umekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa watu wa pande hizo.
Kwa mtazamo wake, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zambia, Chipoka Mulenga, anaona kuwa Maonyesho ya Tatu ya Uchumi na Biashara kati ya China na Afrika ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya China na nchi za Afrika. Anasema fursa hiyo iliyotolewa na China kwa Afrika nan chi nyingine ni kitu ambacho nchi za Afrika zinapaswa kuitumia vizuri kutangaza bidhaa zao na kuingia kwenye soko kubwa la China.
Katika miongo miwili iliyopita, biashara kati ya China na Afrika imeendelea kuongezeka kwa utulivu, na kufikia rekodi ya juu kabisa ya dola za kimarekani bilioni 282 mwaka jana.