Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Masuala ya Kigeni iliyo chini ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Wang Yi, amesema kuwa China, Japan na Korea Kusini zinapaswa kuanzisha tena juhudi za ushirikiano.
Wang Yi amesema hayo katika hotuba aliyotoa kwenye ufunguzi wa Baraza la Kimataifa la Ushirikiano wa Pande Tatu la mwaka 2023 mjini Qingdao, China. Amesema kwa zaidi ya miaka 20, ushirikiano wa pande tatu wa China, Japan na Korea Kusini umekua na kuwa mfumo wenye ushawishi mkubwa katika bara la Asia, na kutoa msukumo muhimu wa kuzifanya nchi hizo tatu za Asia kuwa za kisasa.
Katika mkutano huo, Wang ametoa mapendekezo muhimu matano, ambayo ni kuimarisha kuaminiana, kunufaishana kwa pamoja, kuongeza maingiliano, kusaidiana, na kujifunza kwa pamoja. Pia ametoa wito wa uratibu wa pamoja ili kulinda utulivu na amani ya kikanda, kuanzisha fursa muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi, kuendeleza maingiliano ya kiuchumi ya kikanda, kukabiliana na changamoto kwa pamoja, na kuendelea kuunga mkono masuala yanayohusu jamii katika kanda hiyo.