Wastani wa joto duniani ulifikia kiwango cha juu zaidi siku ya Jumatatu tarehe 3 Julai, na kuzidi nyuzi joto 17 kwa mara ya kwanza. Wanasayansi wanasema namba hizo zilikuwa za juu zaidi katika rekodi zote zilizoanzia mwishoni mwa karne ya 19.
Joto hilo kali linatokana na mchanganyiko wa tukio la hali ya hewa ya El Niño na kuendelea kutoa hewa ya ukaa. Watafiti wanaamini kutakuwa na rekodi za juu zaidi katika miezi ijayo kadri El Niño inavyoimarika.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, watafiti wamekuwa na wasiwasi zaidi juu ya kuongezeka kwa kasi kwa joto la ardhini na baharini. Wiki hii China iliendelea kukumbwa na joto kali na katika baadhi ya maeneo lilifikia juu ya nyuzi 35, wakati Amerika kusini pia kumekuwa na hali mbaya ya joto.
Kiwango cha joto kilichoshuhudiwa Jumatatu ni cha juu zaidi tangu ufuatiliaji wa satelaiti uanze mwaka 1979. Wataalamu pia wanaamini kuwa ni cha juu zaidi tangu kuenea kwa vyombo vya kurekodi mwishoni mwa karne ya 19.