Wajasiriamali wanawake wa Afrika wachangamkia fursa za maonesho ya biashara ya China
2023-07-07 08:56:20| CRI

Maonesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yalifanyika Changsha kuanzia Juni 29 hadi Julai 2. Maonesho haya yamehudhuriwa na makampuni na wafanya biashara mbalimbali wa China na Afrika. Lakini habari njema ni kwamba mwitikio wa wajasiriamali wanawake katika maonesho haya ni mkubwa sana na kuashiria kuwa sasa wanawake wako tayari kushiriki kwenye matukio mbalimbali makubwa ya kimataifa bila uwoga wowote.

Maonyesho ya mwaka huu yalipata mafanikio kadhaa ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Kwani jumla ya miradi 120 ilitiwa saini, yenye thamani ya dola bilioni 10.3. Miradi tisini na tisa ya ushirikiano ilizinduliwa, yenye jumla ya dola bilioni 8.7. Kwa hakika, nchi 11 za Afrika zilichangia idadi hii kwa kuzindua miradi 74, ambayo ni alama ya juu zaidi kufikia sasa.

Maonyesho hayo ya siku nne yalionesha karibu aina 1,600 za bidhaa kutoka nchi 29 za Afrika, ikiwa ni ongezeko kubwa la kustaajabisha la asilimia 166 ikilinganishwa na maonesho ya awali. Tukio hilo lilishuhudia ushiriki wa kina wa wanawake huku kukiwa na jumla ya waoneshaji wapatao 1,500, na kuashiria ongezeko la asilimia 70 yakilinganishwa na maonesho yaliyopita. Uwepo wa wanunuzi 9,000 na wataalamu waliotembelea, uliboresha zaidi mazingira changamfu ya maeonesho hayo, na idadi ya wageni kwa ujumla ilizidi 100,000. Hivyo tukiwa tunaangalia mafanukio ya maonesho hayo, leo tutawazungumzia wajasiriamali wanawake wa Afrika wanavyochangamkia fursa za maonesho ya biashara ya China.