Utafiti: Bara la Afrika kugawanyika, Tanzania kuhusika
2023-07-08 22:51:40| cri

Shirika la Anga ya juu la Marekani (Nasa) kupitia utafiti wake mpya uliochapishwa Juni 2023 umeonyesha dalili za kugawanyika mara mbili Bara la Afrika miaka milioni tano ijayo baada ya bonde la ufa lililopo Kenya na Ethiopia kuzidi kuongezeka.

Taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa ‘Daily Mail’ wa Uingereza inaonyesha mgawanyiko huo unasababishwa na kusukumwa kwa safu kubwa ya mawe yenye joto kali katika kiini cha dunia.

Pia, utafiti huo unaonyesha baada ya Afrika kugawanyika mara mbili nchi za Tanzania, Kenya, Somalia na sehemu ya Ethiopia itaunda bara jipya litakaloongeza idadi ya mabara kutoka saba hadi nane.

Profesa Ken Macdonald wa Chuo Kikuu cha California amesema baada ya Bara la Afrika kugawanyika pia kutaundwa bahari nyingine ambayo itaongeza idadi ya bahari duniani kutoka nne zilizopo hadi tano. Vilevile, katika utafiti wa Nasa unaonyesha ufa wa maili 35 ambao ulionekana mwaka 2005 Ethiopia tayari unaonyesha dalili za bahari mpya karibu katika eneo hilo.