Madai ya Uganda kutopenda Kiswahili ni hadithi za watu tu
2023-07-09 19:52:31| cri

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) James Magode Ikuya, amesema madai kwamba Waganda wana hofu kuhusu kukumbatia Kiswahili ni hadithi tu.

Kinyume chake, nchi hiyo imekuwa ikitumia lugha hiyo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1900 na leo Ijumaa itafanya maadhimisha ya pili ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Akizungumza katika mji wa mpakani wa Namanga wakati wa uzinduzi wa msafara wa amani kote Afrika Mashariki ulioandaliwa na EAC, waziri Ikuya alieleza kuwa Kiswahili kinafanya vyema nchini Uganda sio tu kama chombo cha mawasiliano bali pia katika kuunganisha watu. Aliongeza kuwa dhana kwamba Kiswahili hakina nafasi nchini Uganda ilikuwa ni maneno tu, kinyume na hali halisi mashinani.

Bw Ikuya alisema haikuwa makosa kwa viongozi wa kanda hiyo kukipandisha daraja kutoka lugha ya mawasiliano hadi kuwa lugha rasmi ya EAC. Amedokeza kuwa Kiswahili ndicho chombo bora zaidi cha mawasiliano miongoni mwa jamii mbalimbali za kanda hii hasa zile zinazoishi maeneo ya mipakani.