Rais Xi Jinping wa China amekutana na Waziri Mkuu wa Visiwa vya Solomon Manasseh Sogavare hapa Beijing Jumatatu mchana.
Pande hizo mbili kwa pamoja zilitangaza kuanzishwa rasmi kwa ushirikiano wa kina wa kimkakati wa kuheshimiana na maendeleo ya pamoja kwa zama mpya. Xi alibainisha kuwa China na Visiwa vya Solomon ni marafiki wa kuaminika na washirika wa kutegemeana. Alisema tangu nchi hizo mbili zianzishe uhusiano wa kibalozi, ushirikiano wao wa kirafiki umekuwa chachu ya uhusiano kati ya China na nchi nyingine za visiwa vya Pasifiki licha ya kuchelewa kuanza. Aliongeza kuwa ushirikiano wao ni dhana ya umoja, ushirikiano na maendeleo ya pamoja ya nchi zenye ukubwa tofauti, na kwa nchi zinazoendelea.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Sogavare Alibainisha kuwa uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China ulikuwa chaguo sahihi, na kwamba matokeo yenye manufaa yamepatikana katika uhusiano huo ambapo China imekuwa mshirika mkubwa wa miundombinu ya Visiwa vya Solomon na mshirika wa maendeleo wa kuaminika. Visiwa vya Solomon vinafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na vinapenda kudumisha mawasiliano ya karibu ya kiwango cha juu na China, kuimarisha mabadilishano na ushirikiano katika biashara, uwekezaji, maeneo ya kitamaduni na ya mataifa madogo, na kushughulikia kwa pamoja changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi.