China yafanya mkutano wa ngazi ya juu wa maendeleo ya pamoja
2023-07-11 09:14:03| CRI

Mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu wa Baraza la Hatua za Kimataifa kwa Maendeleo ya Pamoja ulifanyika Beijing jana Jumatatu.

Mkutano huo wenye kaulimbiu "Mpango wa Maendeleo ya Kimataifa: Sisitiza Agenda ya Maendeleo na Wito wa Hatua za Kimataifa." uliandaliwa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa la China.

Ukizingatia maeneo manane muhimu ya ushirikiano chini ya Mpango wa Maendeleo ya Kimataifa (GDI) uliopendekezwa na China, zaidi ya washiriki 800 walijadili na kubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya 2030 na kuhimiza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kwa binadamu.

Katika barua ya pongezi kwa ajili ya mkutano huo, rais Xi Jinping wa China alisisitiza kuwa maendeleo ni kaulimbiu ya milele ya jamii ya binadamu, na maendeleo ya pamoja ni njia muhimu ya kujenga dunia bora. Xi alisema China ikiwa ni nchi kubwa zaidi inayoendelea, daima imekuwa ikiweka maendeleo yake ndani ya muktadha mkubwa wa maendeleo ya binadamu na kutoa fursa mpya za maendeleo ya dunia kupitia maendeleo yake yenyewe.

Naye katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ambaye sasa ni mwenyekiti wa Jukwaa la Boao la Asia, Ban Ki-moon, alisema ni kwa juhudi za pamoja tu ndipo malengo ya maendeleo endelevu yanaweza kufikiwa. Ametoa wito kwa nchi zote kuungana na kuwa kitu kimoja ili kufanya kazi pamoja katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa 2030.