Kenya inatumai kuwa Kiswahili kitakuza biashara, diplomasia ya kitamaduni
2023-07-12 08:45:38| CRI

Mkurugenzi wa diplomasia ya kitamaduni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora, Ann Wanjohi, amesema Kenya itaongeza ustadi wake wa Kiswahili miongoni mwa raia ili kukuza biashara ya kuvuka mipaka na diplomasia ya utamaduni.

Akiongea kwenye shamrashamra za Siku ya Kiswahili Duniani inayoadhimishwa Julai 7 kila mwaka, Wanjohi alisema ni kwa kuwa kituo cha Kiswahili chenye ubora tu, ndio nchi hiyo itakuwa katika nafasi nzuri ya kufanya biashara zaidi na majirani zake na kuongoza juhudi za kikanda za kujenga amani na mafungamano.

Alibainisha kuwa mustakabali wa siku zijazo ni Kiswahili hivyo kama nchi wananuia kukuza lugha ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200, ambapo sasa serikali imetunga sera zinazolenga kukuza Kiswahili kama lugha ya biashara, elimu, burudani, uhusiano wa kidiplomasia na ubunifu.

Shamrashamra hizo zilizoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, zimewaleta pamoja wanadiplomasia, wasomi na wanafunzi ambao walisisitiza ukuaji wa Kiswahili barani Afrika na kwingineko.