Mkurugenzi wa Ofisi ya Idara ya Mambo ya Kigeni ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Wang Yi, Jumanne alikutana na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Jeje Odongo na Burundi Albert Shingiro hapa mjini Beijing.
Akiongea na waziri Odongo Bw. Wang, alisema China itaendelea kuunga mkono maendeleo ya Uganda na juhudi zake katika kuboresha uwezo wa kujitafutia maendeleo yake. Aliongeza kuwa China iko tayari kuimarisha ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Uganda, huku ikitilia maanani nafasi ya Uganda katika masuala ya kimataifa, na kuiunga mkono nchi hiyo katika kulinda uhuru wake, mamlaka yake na ukamilifu wa ardhi yake, pamoja na katika kutekeleza jukumu kubwa zaidi katika masuala ya Afrika.
Aidha alipoongea na waziri Shingiro, Bw Wang aliishukuru Burundi kwa mchango wake chanya katika kufanikisha mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu wa Baraza la Hatua Duniani kwa Maendeleo ya Pamoja, na pia kuishukuru nchi hiyo kwa uungwaji mkono na ushiriki wake katika Mpango wa Maendeleo wa Kimataifa, akisema kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Burundi.