Xi asisitiza uchumi ulio wazi wa hali ya juu na mpito wa nishati
2023-07-12 09:49:48| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesisitiza juhudi za kujenga mifumo mipya ya uchumi ulio wazi wa hali ya juu na kukuza mabadiliko ya taratibu kutoka udhibiti wa kiasi na ukubwa wa matumizi ya nishati hadi udhibiti wa kiasi na ukubwa wa utoaji wa kaboni.

Xi, ambaye pia ni katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na mwenyekiti wa kamati kuu ya jeshi, aliyasema hayo alipokuwa akiongoza mkutano wa kamati ya kuimarisha mageuzi ya kina ya kamati kuu ya CPC anayoiongoza.

Xi amesema kuwa mifumo mipya ya uchumi ulio wazi wa hali ya juu ni hatua ya kimkakati ya kuongeza mageuzi na maendeleo kwa ufunguaji mlango. Amesisitiza umuhimu wa ufunguaji mlango wa kimfumo na kuongeza mageuzi ya kimfumo katika uwekezaji, biashara, mambo ya fedha na uvumbuzi, na maeneo mengine muhimu ya mawasiliano na ushirikiano na nchi za nje, ili kuinua kikamilifu ufunguaji mlango wa China hadi ngazi mpya.

Pia amesema ujenzi wa ustaarabu wa kiikolojia umeingia katika kipindi muhimu ambapo kupunguza uzalishaji wa kaboni imekuwa lengo la kimkakati. Ametaka kufanyika juhudi za kudhibiti kiwango na ukubwa wa matumizi ya nishati na kuhama hatua kwa hatua kuelekea kudhibiti kiwango na ukubwa wa utoaji wa kaboni.