Serikali ya China kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania, umekabidhi vifaa vya michezo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini humo ambavyo vitatumika katika Programu ya Michezo Mtaa kwa Mtaa pamoja na Samia Taifa Cup.
Vifaa hivyo vilivyopokelewa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Dkt. Pindi Chana Jijini Dar es Salaam, ni pamoja na mipira ya Kikapu 600, mipira ya Wavu 600, mipira ya Miguu 600 pamoja na Jezi 2634. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Chana amesema watakabidhi vifaa hivyo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na shule mbili za michezo kwa kila mkoa. Ameongeza kuwa anatumai vifaa hivyo vitawasaidia vijana nchini humo kukuza vipaji vyao na hivyo kuwa msaada kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema nchi yake inaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu wa wataalamu na ujenzi wa miundombinu ya michezo nchini humo.