UM wasema zaidi ya watu 64,000 waingia nchini Ethiopia kutokea Sudan
2023-07-13 21:08:34| cri

Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) limesema idadi ya watu wanaoingia nchini Ethiopia kutokea Sudan imezidi 64,000.

Katika ripoti yake mpya ya hali ya sasa iliyotolewa jana jumatano, IOM imesema mapigano yanayoendelea nchini Sudan yamelazimisha maelfu ya watu kukimbilia katika nchi jirani.

Shirika hilo limesema, mpaka kufikia jumanne wiki hii, zaidi ya watu 64,000 waliingia nchini Ethiopia kupitia maeneo kadhaa ya mpaka wa nchi hiyo katika mikoa ya Amhara, Benishangul, Gumz na Gambella. Pia Shirika hilo limesema limeongeza wafanyakazi wake katika maeneo ya mpakani na kituo cha kupokea wahamiaji kilichoko Metema, na kutoa misaada mbalimbali kwa watu wanaowasili kituoni hapo, ikiwa ni pamoja na msaada wa huduma za afya, maji, afya ya akili na ulinzi.