Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) Jumatano lilisema watu zaidi ya milioni 3 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano nchini Sudan ndani ya muda usiozidi miezi mitatu, ambapo nusu yao wanakadiriwa kuwa ni watoto.
Kwa mujibu wa OCHA, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) liliripoti kuwa watoto takriban milioni 1.5 wamekimbia makazi yao, ingawa baadhi yao bado wako nchini Sudan. Kwa ujumla, mtoto mmoja kati ya watoto wawili yaani takriban watoto milioni 13.6 nchini Sudan wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.
OCHA ilisema tangu mapigano yazuke, UNICEF imetoa vifaa vya matibabu kwa watoto na wanawake zaidi ya milioni 3, na kutoa maji safi ya kunywa kwa watu takriban milioni 1.4. Aidha watoto karibu laki moja wanasoma katika maeneo salama, ikiwa ni pamoja na vituo vya nishati ya jua.