Balozi wa China huko Geneva asema China inapinga aina zote za chuki dhidi ya Uislamu
2023-07-13 09:27:34| CRI

Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa, Balozi Chen Xu amesema China inapinga aina zote za chuki dhidi ya Uislamu.

Akiongea katika mjadala wa kikao cha 53 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) Balozi Chen alisisitiza kuwa China siku zote imekuwa ikihimiza kuheshimiana, kuvumiliana na kuelewana kati ya ustaarabu tofauti.

UNHRC Jumanne ilifungua mjadala wa dharura kuhusu kuongezeka sana kwa vitendo vya chuki za kidini vinavyofanywa hadharani, kama inavyotokea katika baadhi ya nchi za Ulaya ambazo mara kwa mara zinaidhalilisha Qur'ani Tukufu. Baadaye Baraza hilo lilipitisha azimio kuhusu suala hilo Jumatano asubuhi.

Chen amesema China inaunga mkono kufanyika kwa mjadala huo wa dharura na kusisitiza kuwa China inalaani matukio ya kudhalilishwa kwa Qur'ani Tukufu. Alibainisha kuwa huo unaoitwa "uhuru wa kujieleza" haupaswi kutumiwa kama sababu ya kuchochea migongano ya ustaarabu, au kusababisha makabiliano. Balozi Chen amekiambia kikao hicho kuwa, China iko tayari kushirikiana na pande zote katika kutekeleza Mpango wa Ustaarabu wa Kimataifa, unaotetea kuzingatia kanuni za usawa, kujifunza kwa pamoja, mazungumzo na kuvumiliana kati ya ustaarabu.