Ukatili wa kimapenzi ni jambo ambalo limekuwa likipingwa na kuzungumzwa sana, lakini bado matukio ya wanawake ama wakati mwingine wanaume kubakwa yanatokea, hata kwenye ndoa. Baadhi ya wanawake katika ndoa wamekuwa wakitendewa ukatili huu wa kimapenzi, bila ya kujua wapi wapeleke malalamiko yao, na hivyo kujikuta wakiishi maisha ambayo hayana amani, furaha, wala utulivu.
Ukatili wa kimapenzi pia unahusishwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono. Katika sehemu za kazi, taasisi za elimu, biashara, na sehemu nyingi, wanawake wamekuwa wakikumbwa na kadhia ya kuombwa rushwa ya ngono, ili aidha wafaulu masomo, wapate zabuni, ama kupandishwa cheo makazini. Katika kipindi chetu cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tunaangazia suala hili la ukatili wa kimapenzi na rushwa ya ngono na jinsi vinavyoathiri wanawake.