UM wasema watu milioni 783 duniani wakumbwa na njaa mwaka jana
2023-07-16 21:43:50| cri

Mashirika ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni yametoa ripoti ya pamoja ya hali ya lishe na usalama wa chakula duniani ya mwaka 2023 ikisema, mwaka jana watu milioni 783 duniani walikumbwa na njaa, idadi ambayo imeongezeka kwa watu milioni 122 ikilinganishwa na mwaka 2019.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), imesema hali hiyo imetokana na athari za janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya mara kwa mara.

Mashirika hayo yamesema, japo maendeleo ya kupungua njaa yameshuhudiwa katika Asia na Amerika ya Kusini mwaka 2022, lakini tishio la njaa katika Asia Magharibi, eneo la Caribbean na Afrika bado linaongezeka.