Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) Jean Kaseya amesema, Kituo hicho kimetoa kipaumbele katika majibu ya haraka kupambana na magonjwa ya kuambukiza yanayojitokeza, ikiwa ni sehemu ya kuboresha unyumbufu wa mfumo wa afya katika bara hilo.
Akizungumza kando ya mkutano wa uratibu wa katikati ya mwaka wa Umoja wa Afrika uliofanyika mjini Nairobi, Kenya, Kaseya amesisitiza kuwa kudhibiti mzigo mkubwa wa maradhi barani Afrika ni ufunguo wa kutimiza ukuaji na ustawi. Amesema kutokana na mafunzo yaliyopatikana kutoka janga la COVID-19, Kituo chake kinasaidia nchi za bara hilo kutunga mipango ya dharura kwa utayari wa milipuko ya magonjwa katika siku zijazo ili kukwepa vifo vya watu na shinikizo kwa taasisi za afya ya umma.
Pia amesema, Afrika CDC inashirikiana na mashirika ya kikanda kuimarisha utafiti, ufuatiliaji, ripoti, na usimamizi wa magonjwa ya kuambukiza kama Ebola, Malaria, na homa ya Marburg.