Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) kilicho chini ya Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kimeonya kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwa El Nino kutokea katika kanda ya Afrika Mashariki wakati wa msimu wa mvua kati ya mwezi Oktoba na Desemba.
Kituo hicho kimesema, hivi sasa tofauti ya joto katika Bahari ya Hindi (IOD) inayosababisha mvua kubwa, iko katika hali ya kawaida, lakini hali hii itabadilika kuelekea kipindi cha mwezi Oktoba.
Katika taarifa yake, Kituo hicho kimesema kuna uwezekano wa mvua kubwa kunyesha, jambo litakaloleta unafuu kwa maeneo yaliyoathiriwa na ukame, lakini pia mvua hizo zitasababisha matukio mabaya ya hali ya hewa, ikiwemo mafuriko ya ghafla, maporomoko ya matope na maporomoko ya udongo.