Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimetakiwa kupitisha sera zinazohimiza biashara ya ndani ya Afrika katika uzalishaji wa chakula na kuondoa vizuizi visivyo vya ushuru (NTBs).
Haya ni baadhi ya maazimio yaliyopitishwa kwenye Kongamano la 14 la Ngazi ya Juu la Sekta Binafsi la Umoja wa Afrika lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta mjini Nairobi.
Imefahamika kuwa kwa sasa vizuizi visivyo vya ushuru vinafanya uagizaji wa chakula kutoka nje ya bara kuwa wa gharama kubwa, ikilinganishwa na chakula kinachozalishwa ndani. Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika pia zimesisitizwa kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.
Jukwaa hilo pia limezihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kujenga mifumo ya chakula inayostahimili hali ya hewa kwa kutumia teknolojia zinazohimiza uwekezaji ambazo pia hushughulikia hasara baada ya kuvuna.