UNFPA yasema Ethiopia yaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kibinadamu
2023-07-18 08:39:09| CRI

Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) limeonya kuwa Ethiopia inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kibinadamu zinazotokana na majanga ya asili na majanga yanayosababishwa na binadamu.

Katika ripoti yake kuhusu mwitikio wa kibinadamu iliyotolewa jana jumatatu, UNFPA imesema ukosefu wa usalama wa chakula katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo na pia majanga yanayotokana na ukame na mafuriko yamesababisha matishio ya afya na kuongeza wasiwasi juu ya ulinzi.

Shirika hilo limesema, maelfu ya watu wamekosa makazi kutokana na mafuriko katika mikoa kadhaa ya nchi hiyo, na kwamba ingawa wenzi wa kibinadamu wanatoa misaada ya kuokoa maisha ikiwemo makazi, vifaa visivyo vya chakula, maji na huduma za ulinzi, msaada zaidi unatakiwa ili kusaidia watu wengine zaidi katika miezi ijayo ya mwaka huu.

Takwimu zilizotolewa na Shirika hilo zinaonyesha kuwa, watu milioni 20 kwa sasa wanakadiriwa kuwa na uhitaji wa msaada wa kibinadamu nchini Ethiopia.